KWANINI WEMA SEPETU HATUMII UMAARUFU WA DIAMOND KUTAFUTA FURSA YA KUFANYA FILAMU ZAKIMATAIFA?

Siku Diamond Platnumz anafagia tuzo saba za  Kilimanjaro, ubavu wake kushoto Wema Sepetu  alikuwa naye bega kwa bega. Na katika wakati mmoja alipanda jukwaani kutoa maneno ya shukrani kwa niaba yake na alisikika akisema anajivunia kuwa mke mtarajiwa wa staa huyo wa muziki nchini. Wema na Diamond wana historia ndefu ya mapenzi na uhusiano wao unaongoza kwa  kuandikwa zaidi na vyombo vya habari pamoja na kuwa midomoni kwa wapenzi wengi wa muziki  nchini. Kwa pamoja, wana nguvu kubwa ya
ushawishi na kama kweli wakifikia lengo la kuwa mke na mume, wana mustakali mzuri hapo  baadaye. Tunafahamu jinsi Diamond anavyopigana  kujitanua kimataifa na bahati nzuri jitihada zake hazipotei. Mwaka huu peke yake, Diamond amefanikiwa kufanya mambo makubwa kuliko msanii yeyote wa Tanzania. Kuanzia video yake ya My Number One akiwa na Davido kushika  nafasi ya kwanza kwenye runinga kubwa duniani ikiwemo Trace TV,
kutajwa kuwania vipengele  viwili kwenye tuzo za MTV Africa na sasa kutajwa kuwania BET Awards kwenye kipengele cha Best  International Act: Africa.  Kama mambo yakienda vizuri na wengi wakimpigia kura, anaweza kunyakua tuzo moja kati ya hizo. Na ukiangalia, huo ndio kama mwanzo tu wa mafanikio yake, mengi makubwa yanaishiria kumfungulia milango na kukwea juu zaidi. Lakini swali nililonalo kichwani ni je! Wema anautumia umaarufu na fursa aliyoipata mwandani wake kuimarisha kile anachokifanya pia? Wema ni muigizaji wa kike wa filamu mwenye  mashabiki wengi zaidi kuliko wote nchini. Na kwa wale waliokwisha tazama filamu zake, watakubali  kuwa si umaarufu wake tu unaozifanya filamu zake zipendwe, bali ni kweli kipaji cha kuigiza  anacho. Na pengine akiwa chini ya muongozaji  mzuri wa filamu, anaweza kufanya makubwa zaidi katika fani hiyo. Kinachomtofautisha na waigizaji wengine wa Tanzania, ni msingi wa elimu alioupata na hivyo  kuwa na kigezo muhimu wanachokosa waigizaji wengine wa Tanzania ambacho ni uwezo wa  kuongea Kiingereza vizuri. Sijaona jitihada zozote
ambazo mrembo huyu anazifanya kutumia jina la mpenzi wake ambaye kwa sasa nchi nyingi za Afrika zinamfahamu kutengeneza njia na kupata fursa ya kufanya filamu za kimataifa.  Ninachokiona akikifanya Wema kwa sasa, ni kuendelea kufanya kile kile ambacho waigizaji  wengine wa filamu wa Tanzania wanakifanya – kuigiza filamu kwaajili ya soko la ndani. Haoni  kuwa huu ni muda wa yeye kupiga hatua moja
pia? Kuna wakati Wema alikuwa anataka kuelekea huko. Mwaka 2012 alifanikiwa kumdondosha
muigizaji mkubwa wa filamu wa Nigeria, Omotola Jalade kwenye uzinduzi wa filamu ya Supastaa
ambayo hata hivyo haikutoka. Huo ulikuwa mwanzo mzuri wa yeye kujitangaza kwenye  filamu za kimataifa kama ambavyo marehemu Kanumba alikuwa akikifanya kabla ya mauti yake. Nahisi njia nzuri ambayo Diamond angeweza kumsaidia Wema kufanikiwa hilo ni kusafari naye mara kwa mara katika safari zake za kimataifa na huko angekuwa anamuunganisha na wadau muhimu wa fani yake.  Kwakuwa kwa sasa tayari ana jina Nigeria, alikuwa anaweza kumweka karibu na kiwanda cha Nollywood ambacho kwa Afrika ni kikubwa zaidi kibiashara. Alikuwa na uwezo pia wa kumuunganisha na vyuo vizuri kwa masomo ya filamu ambako huko angenoa zaidi uwezo wake wa kuigiza. Kama wanapendana na lengo lao ni kuja kuwa
pamoja, nahisi kuna wakati wanahitaji kuanza kusafiri pamoja na hii inaweza kumfungulia Wema  fursa zaidi kuliko sasa ambapo anaonekana kuridhika na anachokifanya nyumbani.
TOA MAONI YAKO HAPO CHINI
BOFYA “LIKE” HAPO CHINI KUPATA HABARI ZETU..!!

0 comments: