HIZI NDIZO SABABU ZA KIFO CHA MSANII ADAM KUAMBIANA..!! SOMA HAPA KUZIJUA
KWELI kifo
hakina huruma! Msemo huu umetimia juzi kufuatia kifo cha ghafla cha
mwigizaji na mwongozaji wa filamu za Kibongo, Adam Philip Kuambiana (38)
kilichotokea akiwa njiani kukimbizwa kwenye Hospitali ya Mama Ngoma,
Mwenge jijini Dar es Salaam baada ya kuugua.
Kuambiana
aliugua ghafla kwenye kambi ya kurekodi filamu na wasanii wenzake
iliyopo katika Nyumba ya Kulala Wageni ya Silvarado iliyopo Sinza ya
Kwaremmy, Dar.
NINI CHANZO CHA KIFO?
Akizungumza na
Ijumaa Wikienda Jumamosi iliyopita nje ya Hospitali ya Mama Ngoma,
msanii wa Bongo Fleva, Aboubakar Katwila ‘Q-Chillah’ alisema muda
mchache kabla ya kufikwa na mauti, Kuambiana alimlalamikia maumivu ya
tumbo ambapo Ijumaa iliyopita alisema hali yake si nzuri kwani alikuwa
akiendesha damu tupu.
Q-Chillah
alisema: “Jana (Ijumaa) jioni Kuambiana na wasanii wenzake walikuwa baa
wakinywa pombe hadi usiku mnene lakini bado aliendelea kulalamikia
maumivu ya tumbo.
“Wenzake walimuuliza ni kwa nini alikuwa akiendelea kunywa pombe kama anaumwa? Akawaambia wamuache!
“Baada ya
kumaliza kunywa kila mmoja alikwenda kulala chumbani kwake huku
tukiahidiana kwamba itakapofika saa 3:00 asubuhi tuwe tayari kwa ajili
ya kwenda ‘location’.
“Lakini ulipofika muda huo sisi tukiwa tayari kwa safari tulikwenda kugonga mlango wa chumba chake bila mafanikio.
“Cha
kushangaza, alisikika sauti yake kwa mbali. Kwa bahati nzuri mlango
ulikuwa wazi, mmoja akaingia ndani na kumkuta ameanguka chooni na
hajiwezi. Neno lake la mwisho alisema kwamba anajisikia kuishiwa nguvu
na anaharisha damu.
“Kutokana na
hali yake hiyo mbaya tulimbeba na kumlaza kitandani kisha tukatafuta
gari na kumkimbiza Hospitali ya Mama Ngoma ambapo daktari alisema kwamba
alishafariki dunia muda mrefu.”
VIDONDA VYA TUMBO VYATAJWA
Kwa mujibu wa
watu wa karibu, Kuambiana kwa muda mrefu amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa
wa vidonda vya tumbo (ulcers). Lakini pia inadaiwa alikuwa akisumbuliwa
na kisukari (diabetes).
DAKTARI AELEZEA
Ijumaa
Wikienda lilimtafuta daktari mmoja wa Hospitali ya Taifa Muhimbili
(aliomba jina kuhifadhiwa) ili azungumzie kuhusu vidonda vya tumbo,
alisema:
“Kwa kawaida,
mtu kuharisha damu kwa sababu ya vidonda vya tumbo inawezekana kabisa,
hiyo kitaalam inaitwa heamatemesis. Inatokana na perforation ya tumbo
yaani kidonda kuwa kikubwa.
“Kwa mtumiaji
wa pombe ni kipindi anatakiwa kusimama au kuacha moja kwa moja. Kama
hatajali afya yake anaweza kufa ghafla kwani uwezekano wa utumbo
kukatika ghafla ni mkubwa.”
Msanii wa Muziki wa Kizazi Kipya, Aboubakar Katwila ‘Q-Chillah’ na msanii aliyekuwa akishuti video pamoja na Kuambiana muda mfupi kabla ya kifo wakiwa katika majonzi.
ALIJUA KIFO CHAKE
Q-Chilla
ambaye ni miongoni wa wasanii wanaocheza filamu hiyo, aliendelea kusema
kuwa siku chache kabla ya kifo, Kuambiana alimwambia filamu yake hiyo
inayoitwa Jojo ndiyo ya mwisho, hatajishughulisha tena na sanaa na
alikuwa na mpango wa kwenda China kupumzika kwa muda mrefu.
“Nimeumia sana
kwani hii filamu ndiyo ilikuwa apate fedha nyingi sana kwa sababu ni ya
kwake mwenyewe na ni kali mno, amecheza vizuri akinishirikisha mimi.
“Lakini ndiyo
hivyo tena imeishia katikati, sijui ni nani atakayeiendeleza maana
mwenyewe katuachia majonzi yasiyoelezeka,”alisema Q-Chillah.
AMEMFUATA MDOGO WAKE
Habari zaidi
zinasema kwamba, Kuambiana ameaga dunia hata arobaini ya mdogo wake wa
damu, Patrick haijafika. Patrick alifariki dunia mwezi mmoja uliopita.
AKUTANA NA MHARIRI WA GLOBAL
Ijumaa saa
10:00 jioni maeneo ya Sinza Kwaremmy jirani na Silvarado, Kuambiana
alikutana na Mhariri Kiongozi wa Magazeti Pendwa ya Global Publishers,
Oscar Ndauka.
Mhariri huyo alimuuliza ni kwa nini hawaonani siku hizi, Kuambiana akajibu:
“Nipo Mr
Ndauka, nipo bwana. Tutaonana lakini sina hakika sana.” Kuambiana
alionekana mwenye afya njema na alimtania mhariri huyo kwa kumwambia:
“Naona siku hizi Ndauka unazidi kunenepa tu, mi maisha yananipiga.”
STEVE NYERERE, BATULI WALIA SANA
Baada ya
taarifa kuenea, wasanii mbalimbali wa filamu walikusanyika katika
Hospitali ya Mama Ngoma ambapo Mwenyekiti wa Bongo Movie Unity, Steven
Mengere ‘Steve Nyerere’ na Yobnesh Yusuf ‘Batuli’ walivunja rekodi ya
kulia kufuatia kifo hicho.
WADAU WAZUNGUMZIA MTU KUANGUKA CHOONI
Wadau na
mashabiki wa filamu waliokuwa eneo hilo walisikika wakisema kwamba
wasanii wengi hawana tabia za kucheki afya zao, jambo ambalo
linawagharimu kiasi cha kupoteza maisha.
Wengine walisikika wakisema kwamba watu wanaoanguka chooni mara nyingi huwa hawaponi, wakipona huwa wanapooza miili.
“Unajua watu
wengi wanakosea, pale mtu anapodondoka chooni wanamkimbiza hospitali
badala ya kumtibu kienyeji, mtu akianguka chooni tu anatakiwa kupewa
ndizi mbivu lakini akipelekwa hospitali lazima afe,” walisikika watu.
HISTORIA YAKE KWA UFUPI
Marehemu Kuambiana alizaliwa mwaka 1976, Ifunda mkoani Iringa. Kabila ni Mmakua wa mkoani Mtwara.
Marehemu Kuambiana anatarajiwa kuzikwa kesho kwenye Makaburi ya Kinondoni jijini Dar.
Mungu ailaze pema peponi roho yake. Amina.
0 comments: