MUHIMU..!! KWA WAKAZI WA JIJI LA DAR ES SALAAM , NAULI ZA DALADALA SASA KUPANDA HADI Tsh. 800/=
atimaye picha halisi ya gharama ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam
(Dart) awamu ya kwanza, imeonesha nauli ya basi kutoka maeneo
mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam kwenda na kurudi vituo vikubwa
vikiwemo vya Kariakoo na Posta, itapanda kutoka nauli ya chini ya Sh 400
ya sasa mpaka Sh 700 na Sh 800 kwa ruti moja.
Kwa wanafunzi, nauli kwa ruti moja
kwenda katika vituo hivyo vikubwa katika mradi huo ambao utaanza kwa
majaribio mwishoni mwa mwaka huu, zitapanda kutoka Sh 200 mpaka nusu ya
nauli ya mtu mzima kwa ruti husika.
Aidha, mfumo wa uendeshaji wa mradi huo
na nauli, umewekwa katika sehemu mbili; sehemu ya kwanza ni usafirishaji
wa abiria kutoka maeneo ya ndani ya makazi ya watu mpaka katika vituo
vidogo na vikubwa vilivyopo barabara kuu za Dart, za Morogoro na Kawawa
kwa sasa na sehemu ya pili ni usafirishaji wa abiria kutoka katika vituo
vilivyopo katika barabara kuu ya Dart za Morogoro na Kawawa, kwenda
vituo vikuu vikiwemo Kariakoo na Posta.
Hayo yamebainishwa jana jijini Dar es
Salaam, katika taarifa ya mwisho ya Makubaliano ya Dart, iliyotolewa
katika mkutano wa Mashauriano ya Uwekezaji wa awamu ya kwanza ya mradi
huo wa Dart.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa, abiria atakayelazimika kusafiri na mabasi ya Dart kwa safari
fupi ndani ya barabara zilizo katika makazi ya watu, kwa mfano wa
barabara inayopita Sinza; kutoka Bamaga mpaka Shekilango, atalipa Sh
500, tofauti na sasa ambapo analipa Sh 400.
Kwa atakayetumia mabasi ya Dart kutoka
katika barabara ndogo zilizopo katika makazi ya watu, kwenda katika
vituo vikubwa vya Dart vilivyopo njia kuu za Morogoro na Kawawa ili
kwenda Kariakoo, Posta au Kimara, atalazimika kukata tiketi ya Sh 800,
atakayoitumia kupata usafiri kutoka barabara ndogo na katika barabara
kubwa.
Mfano wa nauli hiyo, ni abiria anayetoka
maeneo hayo ya Sinza kwenda Kimara, Kariakoo au Posta, ambaye
atalazimika kukata tiketi ya Sh 800, itakayomwezesha kupakia basi la
Dart kutoka maeneo hayo mpaka Shekilango, ambako atabadilisha basi kwa
tiketi hiyo hiyo, kwenda Kariakoo, Posta au Kimara.
Aidha kwa abiria watakaolazimika kutumia
mabasi matatu ya Dart, kutoka katika barabara ndogo zilizopo katika
makazi ya watu, kupitia barabara kuu za Dart na kwenda katika eneo
lililopo katika barabara ndogo za makazi ya watu, watalazimika kulipa Sh
900 kwa mabasi yote matatu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mabasi
yatakayotumika kubeba abiria kwenye njia kuu, yatachukua watu zaidi ya
150 kwa basi moja, ambapo abiria watakaopata viti vya kuketi ni 52 na
wengine wamewekewa eneo nadhifu la kusimama.
Kwa mabasi yatakayobeba abiria kutoka
njia ndogo zilizopo katika makazi ya watu, yatachukua watu zaidi ya 80,
kati ya hao abiria 42 ndio watakaopata nafasi ya kukaa na waliobakia
wamewekewa nafasi nadhifu ya kusimama.
Kuhusu muda utakaotumika kwenye ruti
moja ya mabasi hayo ya Dart, abiria atatumia muda wa dakika zisizozidi
30 kufika anakokwenda, akitumia mabasi kwenye njia kuu, tofauti na sasa
ambapo kwa kutumia daladala abiria hutumia zaidi ya saa mbili kufika
waendako.
Akizungumza katika mkutano huo, Katibu
Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), Jumanne Sagini, utaratibu wa ulipaji nauli kwenye mabasi ya
Dart, utakuwa ni wa kutumia mfumo wa kadi ambapo abiria anatakiwa anunue
tiketi kabla ya safari.
Alisema utaratibu huo, utapunguza au
kuondoa kero kwa abiria na katika mabasi madogo yanayobeba abiria
kuwaunganisha kwenye njia kuu, yatakuwa na vifaa vya mawasiliano baina
ya dereva aliye barabara ndogo na dereva aliye barabara kuu za Dart.
Kwa mujibu wa Sagini, mradi huo ukianza, abiria watanunua tiketi kwa kupitia huduma za fedha kwa njia ya simu kama vile M-pesa, Tigo-pesa, Pesa Fasta na Airtel Money.
Alisema ili kuzuia wizi na udanganyifu kwenye vituo vya mauzo ya tiketi na kwenye vituo vya mabasi, zinafungwa kamera na video ili kuimarisha ulinzi, na kuhakikisha mapato halali kwa ruti zinazofanywa.
“Hii itasaidia kuondoa wizi na uhujumu unaoweza kufanywa katika vituo vya abiria,” alisema Sagini.
Alisema kwa hatua hiyo, dalaldala za
sasa zitaondolewa katika zaidi ya njia 43 ambazo ziko kwenye barabara ya
Morogoro na barabara ya Kawawa na katika ruti nyingine, daladala hizo
zitaendelea kuondolewa hadi hapo ujenzi wa barabara zote za Dart
utakapokamilika.
Katika mabasi hayo ya kubeba abiria
kwenye njia kuu za Dart, mabasi yanayoruhusiwa ni yale yatakayokidhi
vigezo, ambavyo ni pamoja na kuwa na upana wa meta 18 na uwezo wa kubeba
abiria 150, ambayo yanahitajika mabasi 145.
Kwa mabasi yatakayosogeza abiria hadi
njia kuu, yatatakiwa yawe na uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 80 na upana
wa meta 12 na yatatakiwa mabasi 90.
Akitoa mwito kwa wawekezaji wa ndani na
nje, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia, alisema ni vyema katika sekta binafsi,
wadau wa usafiri na watu mbalimbali wachangamkie fursa hiyo.
Alisema Serikali kupitia mfumo wa ushirikishaji sekta binafsi, umeona ni vyema kushirikisha wadau hao kwenye mradi huo mkubwa Afrika Mashariki, ambao ukitumika vizuri ni chachu ya maendeleo na ukuaji uchumi.
0 comments: